Polisi ya Nigeria yaua 'majambazi' 100 jimboni Zamfara
Polisi ya Nigeria imedai kuwa imefanikiwa kuwaangamiza majambazi 100 katika operesheni iliyofanyika katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi.
Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Jimoh Moshood, Msemaji wa Polisi ya Nigeria ambaye ameongeza kuwa, majambazi hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliuawa katika operesheni iliyofanyika Alkhamisi.
Hata hivyo Isa Sanusi, Msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International amesema ni vigumu kuzungumzia mafanikio ya operesheni hiyo, kwa kuwa mara nyingi taarifa zinazotolewa na maafisa usalama huwa zinakinzana na hali halisi katika maeneo ya tukio, na sio ajabu aghalabu ya waliouawa katika operesheni hiyo ya Zamfara ni raia wa kawaida.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya askari wapatao 100 wa jeshi la Nigeria kuuawa katika shambulio dhidi ya kituo cha jeshi kwenye kijiji cha Metele katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa, ambapo duru za usalama zilisema, lilifanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu Afrika Magharibi, lililojitenga na Boko Haram.
Boko Haram ni kundi linalofuata itikadi za Kiwahhabi na limeitumbukiza Nigeria katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha mizozo ya kidini na kikabila nchini humo.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ambaye kwa sasa yuko katika kampeni za kugombea kiti hicho kwa muhula wa pili katika uchaguzi wa Februari mwakani, anakabiliwa na changamoto nyingi, haswa ukosefu wa usalama.