Misri yamteua mkuu mpya wa intelijinsia wa jeshi
Misri imemteua Meja Jenerali Khalid Megawer kuwa Mkuu Mpya wa Intelijinsia wa Jeshi la nchi hiyo. Nafasi hiyo awali ilikuwa ikishikiliwa na Mohamed al Shahat.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, jeshi na idara ya intelijinsia ya Misri zimekuwa na nafasi kuu katika uchukuaji maamuzi ya juu serikalini tangu rais wa sasa wa nchi hiyo Abdel Fattah al Sisi aongoze jeshi kumpindua madarakani rais wa wakati huo wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Mohamed Morsi kutoka Harakati ya Ikhwanul Muslimin. Hakuna maelezo yaliyotolewa na duru za habari kuhusu sababu iliyopelekea kuuzuliwa al Shahat, hata hivyo Rais al Sisi katika miaka ya karibuni amefanya mabadiliko kadhaa katika safu ya maafisa wa usalama wa ngazi za juu jeshini, katika Wizara ya Mambo ya Ndani na wa idara kuu ya intelijinsia ya nchi hiyo .
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni mwaka huu Rais wa Misri alimteua muitifaki wake wa karibu Meja Jenerali Abbas Kamel kuwa Mkuu wa Idara Kuu ya Intelijinsia ya nchi hiyo wiki mbili baada ya kuwabadilisha Mawaziri wa Ulinzi wa Mambo ya Ndani.
Kabla ya uteuzi huu mpya, Meja Jenerali Khalid Megawer alikuwa Naibu wa Idara ya Intelijinsia ya Jeshi na Mwambata wa Masuala ya Ulinzi katika Ubalozi wa Misri mjini Washington, Marekani.