Essebsi: 2019 ni mwaka muhimu kwa Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50569-essebsi_2019_ni_mwaka_muhimu_kwa_tunisia
Rais wa Tunisia amezungumzia uchaguzi ujao wa rais na bunge nchini humo na kusema kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka muhimu kwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 01, 2019 23:17 UTC
  • Essebsi: 2019 ni mwaka muhimu kwa Tunisia

Rais wa Tunisia amezungumzia uchaguzi ujao wa rais na bunge nchini humo na kusema kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka muhimu kwa nchi hiyo.

katika ujumbe wake mwaka mpya wa 2019, Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisiai ameeleza kuwa jitihada kubwa zinapaswa kufanyika kuandaa mazingira bora ya kufanyika uchaguzi wa wazi, huru na wa kidemokrasia katika mwaka huu wa 2019. 

Rais Tunisia amewataka wananchi wa nchi hiyo kutumia haki yao ya kikatiba na  kushiriki kwenye chaguzi hizo. Vilevile amewataka Watunisia kuwachagua watu wanaofaa kwa ajili ya kushika nyadhifa za kuiongoza nchi hiyo. Rais wa Tunisia ameongeza kuwa mwaka 2018 ulikuwa mwaka mgumu kwa nchi hiyo kutokana na maandamano ya wananchi, ghasia, mashinikizo ya kiuchumi, kuongezeka idadi ya watu wasio na ajira na kupungua sana uwezo wa kifedha wa wananchi wa kununua bidhaa muhimu. Tunisia kwa siku kadhaa sasa imekumbwa na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali yaliyopewa jina la "Vizibao Vyekundu". Maandamano hayo yamepata mwamko kutokana na yale ya nchini Ufaransa ya harakati ya "Vizibao vya Njano."

Wanaharakti wa Vizibao Vyekundu wakiandamana dhidi ya serikali 

Wanaharakati wa Vizibao Vyekundu nchini Tunisia wanasema kuwa wataendelea kufanya maandamano wakilalamikia utendaji wa serikali na hali mbaya ya uchumi nchini humo. Wafanya maandamano hao wanataka serikali itekeleze baadhi ya marekebisho ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi.