Buhari: Jeshi litakabiliana vikali na hatua za kukwamisha uchaguzi ulioakhirishwa
(last modified Tue, 19 Feb 2019 07:53:30 GMT )
Feb 19, 2019 07:53 UTC
  • Buhari: Jeshi litakabiliana vikali na hatua za kukwamisha uchaguzi ulioakhirishwa

Rais Muhammadu Buhari ametahadharisha kuwa yoyote anayejaribu kuzuia uchaguzi wa rais ulioakhirishwa nchini humo anahatarisha maisha yake. Rais wa Nigeria ameituhumu pia Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kwa kutofanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Tume ya Uchaguzi ya Nigeria (INEC) ilitangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais mapema Jumamosi wiki hii; wakati wananchi wa Nigeria wasiopungua milioni 84 walipokuwa wakielekea kwenye vituo vya kupigia kura. Rais wa Nigeria amesema kuwa yoyote anayejaribu kuiba au kupoteza masanduku ya kupigia kura na vifaa vya uchaguzi kwa ujumla katika uchaguzi huo ambao sasa umepangwa kufanyika Jumamosi ijayo atakabiliwa ipasavyo.

Wananchi wakitoa maoni yao baada ya kuakhirishwa uchaguzi wa rais

Amesema ameliagiza jeshi la polisi kuwa wakali. Amesema yeyote mwenye lengo la kuvuruga au kuingilia kati uchaguzi huo ujao atakuwa ameyaweka maisha yake hatarini. Hii ni katika hali ambayo chama tawala na upande wa upinzani zimenyosheana kidole cha lawama kufuatia kuakhirishwa uchaguzi huo. Chama kikuu cha upinzani Nigeria PDP kinasema kuwa Buhari mtawala wa zamani  wa kijeshi nchini humo anahusika katika kuakhirishwa uchaguzi huo wa rais ili kusalia madarakani. Nacho chama tawala  kimekituhumu chama hicho cha upinzani kuwa kimehusika katika njama hiyo kikisema kuwa kinashirikiana na maafisa wa tume hiyo ya uchaguzi.

 

 

Tags