Mar 24, 2019 14:57 UTC
  • WHO yaomba msaada kimataifa kukabiliana na Ebola DRC

Shirika la Afya Duniani WHO limetoa wito wa kukabiliana na hali ya mlipuko wa homa ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ambako watu takriban 1,000 wameambukizwa ugonjwa huo.

Tangu homa ya Ebola ilipolipuka nchini humo mwezi Agosti mwaka 2018, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa au wanaoshukiwa kuambukizwa imefikia 993, na 621 kati yao wamefariki.

Taarifa ilyoitolewa na WHO imetahadharisha kwamba ingawa watu zaidi ya elfu 96 nchini humo wamepata chanjo, na watu zaidi ya milioni 44 wamepimwa wanapovuka mipaka, bado kuna hatari kubwa kwa Ebola kuenea nchini humo na katika kanda hiyo, hasa mapambano na vurugu zitakapotokea.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema WHO ina jukumu la kuwafanya watu wa Kivu Kaskazini washikamane, ili kumaliza mlipuko wa ugonjwa huo, kujenga mfumo wa afya, na kuondoa tishio la afya linalowakabili kila siku.

Chanjo wa Ebola

Hadi kufikia tarehe 27 Novemba 2018, kulikuwa kumeripotiwa kesi 422 za Ebola, 375 kati ya hizo zikiwa zimethibitishwa na 47 ni za kudhaniwa. Hadi tarehe hiyo, watu 242 walisharipotiwa kufariki dunia huko Kivu Kaskazini na Ituri. Mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

 

Tags