Watu 60 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Burkina Faso
Watu wasiopungua 60 wameuawa katika mapigano ya kikabila kaskazini mwa Burkina Faso.
Serikali kupitia msemaji wa chama tawala cha Movement of People for Progress (MPP), Bindi Ouoba imesema hayo katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano na kuongeza kuwa, mauaji hayo ya kikabila yamefanyika ndani ya siku chache zilizopita.
Bindi Ouoba amebainisha kuwa, wimbi jipya la mapigano ya kikabila liliripuka baada ya kiongozi wa kidini pamoja na watu sita wa familia yake kuuliwa na watu wasiojulikana karibu na mji wa Arbinda, katika mkoa wa Soum usiku wa kuamkia Jumatatu.
Naye waziri wa kieneo, Simeon Sawadogo jana usiku aliiambia kanali ya televisheni ya serikali kuwa, watu 62 wameuawa katika mapigano hayo mapya katika mji wa Arbinda, na kwamba 30 waliuawa katika makabiliano ya kikabila huku 32 wakiuawa katika shambulio la kigaidi.
Mapema mwaka huu, zaidi ya watu 40 waliripotiwa kuuawa katika mapigano mengine ya kikabila kaskazini mwa Burkina Faso, hali ambayo ilisababisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kutoa taarifa ya kulaani ghasia hizo.
Mbali na mauaji ya kikabila, Burkina Faso kama zilivyo nchi nyingine za eneo la Sahel imekuwa ikishuhudia mashambulio ya magenge ya kigaidi yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.