Jeshi la Sudan lasema halitamkabidhi Omar al-Bashir kwa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52809-jeshi_la_sudan_lasema_halitamkabidhi_omar_al_bashir_kwa_icc
Baraza la Kijeshi la Mpito linaloshikilia hatamu za uongozi nchini Sudan limepuuzilia mbali mwito wa kumkabidhi Omar al-Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likisisitiza kuwa yumkini rais huyo aliyeng'olewa madarakani akafunguliwa mashitaka nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 12, 2019 20:46 UTC
  • Jeshi la Sudan lasema halitamkabidhi Omar al-Bashir kwa ICC

Baraza la Kijeshi la Mpito linaloshikilia hatamu za uongozi nchini Sudan limepuuzilia mbali mwito wa kumkabidhi Omar al-Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, likisisitiza kuwa yumkini rais huyo aliyeng'olewa madarakani akafunguliwa mashitaka nchini humo.

Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Omar Zeinalabdin, Mkuu wa Kamati ya Kisiasa wa baraza hilo la kijeshi ambaye alibainisha kuwa, "Sisi kama Baraza la Kijeshi, katika taratibu zetu hatuwezi kumkabidhi rais ili akafunguliwe mashitaka nje ya nchi, huenda tutamshitaki hapa, lakini kumkabidhi nje ya nchi hatuwezi kabisa."

Baraza hilo limetoa taarifa hiyo masaa machache baada ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuitaka serikali ya mpito ya Sudan itoe ushirikiano kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, ambayo imetoa waranti wa kukamatwa Omar al-Bashir, rais wa Sudan aliyelazimika kujiuzulu hivi karibuni kufuatia maandamano ya wananchi. 

Msemaji wa ofisi hiyo ya UN, Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, "Tunawaasa viongozi wa Sudan kushirikiana kikamilifu na kutoa usaidizi unaohitajika na ICC, kwa kuzingatia kuwa kuna azimio la Baraza la Usalama la umoja huo la mwaka 2005 linaloitaka serikali ya Khartoum ishirikiane na mahakama hiyo."

 

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

Aidha hapo jana, Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alitoa mwito kwa vyombo vya dola nchini Sudan kuwaachia huru watu wanaozuiliwa kwa kushiriki maandamano ya amani tangu Disemba mwaka jana, sanjari na kuchunguza utumiaji wa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao.

Al Bashir anatuhumiwa na ICC kuwa alihusika na jinai na mauaji ya kimbari huko Darfur magharibi mwa nchi hiyo mwaka 2003.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi imetoa waranti wa kukamatwa al-Bashir mara mbili, mwaka 2009 na 2010. Hata hivyo nchi nyingi hususan za Afrika zilikataa kumkamata na kumkabidhi kwa ICC mtawala huyo aliyeiongoza Sudan kwa miaka 30, alipozitembelea nchi hizo.