Viongozi wa maandamano Sudan wasimamisha mazungumzo na jeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53013-viongozi_wa_maandamano_sudan_wasimamisha_mazungumzo_na_jeshi
Viongozi wa maandamano ya wananchi nchini Sudan wamesema wamesimamisha mazungumzo na Baraza la Mpito la Kijeshi huku wakitoa wito kwa Wasudan kuendeleza maandamano nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum na miji mingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2019 02:52 UTC
  • Viongozi wa maandamano Sudan wasimamisha mazungumzo na jeshi

Viongozi wa maandamano ya wananchi nchini Sudan wamesema wamesimamisha mazungumzo na Baraza la Mpito la Kijeshi huku wakitoa wito kwa Wasudan kuendeleza maandamano nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum na miji mingine.

Msemaji wa harakati ya waandamanaji Mohamed al Amin alitangaza uamuzi huo wakati alipowahutubia maelfu ya waandamanaji nje ya makao makuu ya jeshi. Amesema wanalitazama Baraza la Mpito la Kijeshi kuwa sehemu ya utawala wa Omar la Bashir aliyepinduliwa.

Amin amesema waandamanaji wataelendelea na maandamano hadi pale jeshi litakapotekeleza takwa lao la kutaka baraza la kiraia lishikilie madaraka kwa muda.

Wakati huo huo mapema jana Jumapili Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi Abdel Fattah al-Burhan alisema yuko tayari kuwakabidhi madaraka wananchi huku akisema atajibu matakwa yao katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Omar al Bashir

Itakumbukwa kuwa, Rais Omar al-Bashir alipinduliwa mnamo Aprili 11 baada ya maandamano ya miezi mitatu ya wananchi; na hivi sasa  Baraza la Kijeshi la Mpito chini ya uongozi wa  Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan Abdelrahman limechukua madaraka kwa muda.