Apr 28, 2019 01:15 UTC
  •  Ugonjwa wa Ebola umeua watu 900 DRC tokea Agosti 2018

Ugonjwa wa Ebola umeua watu wapatao 900 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) tokea uibuke Agosti mwaka 2018.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo , idadi kubwa zaidi ya watu wamepoteza maisha katika eneo la Katwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Aidha hadi sasa watu zaidi ya 1,400 wameripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo kote DRC. Hali ya usalama katika mkoa huo imepelekea iwe vigumu sana kudhibiti ugonjwa huo hatari wa Ebola.

Katika taarifa siku ya Alhamisi, Shirika la Afya Duniani WHO lilisema kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la ukosefu wa usalama katika maeneo ya Butembo na Katwa na hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wa afya wanaowashughulikia watu walioambukizwa Ebola.

Chanjo ya Ebola

Hivi karibuni kundi la wanamgambo lilishambulia kituo kimoja cha afya huko Butembo ikiwa ni masaa machache tu baada ya shambulio jingine kama hilo lililopelekea daktari mmoja kutoka Cameroon kuuawa. Kufuatia hali hiyo ya kukosekana usalama, madaktari wanaofanya juhudi za kuwatibu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaougua maradhi ya Ebola wametishia kufanya mgomo endapo watashambuliwa tena.

Wataalamu wa afya wanasema hakuna dalili za ugonjwa wa Ebola kupungua DRC bali kinachotazamiwa ni kuwa ugonjwa huo utazidi kuenea. 

 

Tags