Kiongozi wa upinzani Sudan ataka nchi hiyo ijiunge na ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53134-kiongozi_wa_upinzani_sudan_ataka_nchi_hiyo_ijiunge_na_icc
Kiongozi wa upinzani nchini Sudan amesema nchi hiyo inapaswa kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mara moja.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 27, 2019 23:20 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Sudan ataka nchi hiyo ijiunge na ICC

Kiongozi wa upinzani nchini Sudan amesema nchi hiyo inapaswa kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mara moja.

Kiongozi wa chama cha Umma Sadiq al-Mahdi amesema nchi yake inapaswa kujiunga na mahakama hiyo yenye makao yake The Hague na ambayo inamsaka rais wa Sudan aliyepinduliwa Omar al Bashir kutokana na jinai za kivita alizotenda.

Al-Mahdi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema kujiunga na ICC kunapaswa kufanyika kwa ushirikiano na Baraza la Mpito la Kijeshi ambalo lilichukua madaraka baada ya al Bashir kupinduliwa hivi karibuni.

ICC imetoa waranti wa kukamatwa al Bashir kutokana na nafasi yake katika jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari wakati wa mgogoro wa eneo la Darfur nchini humo.

Sadeq al Mahdi

Al Bashir 75, alipinduliwa na jeshi la Sudan Aprili 11 baada ya miezi mitatu ya maandamano ya wananchi ambapo jeshi lilitangaza kuwaunga mkono wananchi na hivyo kuhitimisha utawala wake wa miaka 30.

Al-Mahdi amesema chama chake kitafikia muafaka na Baraza la Mpito la Kijeshi kuhusu kuundwa baraza la kiraia ili kuongoza nchi hiyo.

Siku ya Ijumaa maelfu ya wananchi wa Sudan waliswali Swala ya Ijumaa nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum, siku moja baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa katika kona mbalimbali za mji mkuu huo, kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Wananchi wa Sudan wanalitaka jeshi hilo liharakishe mchakato wa kukabidhi madaraka kwa raia.