Wapinzani Sudan: Baraza la Kijeshi linafanya jitihada za kung'ang'ania madaraka
Makundi ya kisiasa nchini Sudan yamelituhumu Baraza la Kijeshi la Mpito kwamba linakusudia kuendelea kushikilia madaraka kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa nchi hiyo.
Katika hali ambayo maandamano na migomo nchini Sudan bado inaendelea, shakhsia kadhaa na Muungano Huru wa Mabadiliko wametangaza kwamba, baraza hilo la mpito linafanya jitihada kupitia shughuli zake za kiraia, liweze kuchukua nafasi ya uongozi wa nchi hiyo. Aidha wapinzani sambamba na kusisitizia upinzani wao dhidi ya utawala wa Baraza hilo la Kijeshi la Mpito wametahadharisha kwamba wanafuatilia machaguo walionayo ili kuweza kufikia malengo yao.
Hii ni katika hali ambayo Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika Jumanne iliyopita lilitangaza kulipatia baraza hilo la kijeshi muda wa siku 60 liwe limekabidhi uongozi kwa raia, la sivyo lisimamishe uanachama nchi hiyo katika bara hilo. Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika lina jukumu la kusimamia usalama na uthabiti ndani ya bara hilo. Itakumbukwa kuwa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan lilichukua uongozi wa nchi hiyo baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Omar Hassan al-Bashir, suala ambalo limewatia wasi wasi mkubwa Wasudan.