Wapinzani nchini Sudan: Baraza la Mpito la Kijeshi linapoteza muda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53366-wapinzani_nchini_sudan_baraza_la_mpito_la_kijeshi_linapoteza_muda
Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamelituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2019 02:52 UTC
  • Wapinzani nchini Sudan: Baraza la Mpito la Kijeshi linapoteza muda

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamelituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Viongozi wa maandamano ya Sudan wametishia kuanzisha maandamano ya kitaifa sambamba na kususia shughuli zote za serikali endapo watawala wa kijeshi wataendelea kufanya njama za kupoteza muda na kutokabidhi uongozi wa nchi kwa utawala wa kiraia. 

Waandamanaji hao wanasisitiza kwamba, Baraza la Mpito la Kijeshi linapaswa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia kama lilivyoahidi.

Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.

Viongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi nchini Sudan

Baraza la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Baraza hilo lina wajumbe 9 wakiwemo wanajeshi sita, polisi wawili na afisa mmoja wa masuala ya kijasusi na usalama wa taifa.

Hivi karibuni, baraza hilo la kijeshi nchini Sudan lilikataa pendekezo la kamati ya upatishi kuhusu muundo wa Baraza la Utawala litakalokuwa na wanajeshi watatu na raia saba kwa ajili ya kuongoza kipindi cha mpito, likisisitiza kwamba, muundo unapaswa kuwa na uwiano yaani wanajeshi watano na raia watano.