Nchi za Afrika zatakiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50
(last modified Thu, 09 May 2019 12:40:34 GMT )
May 09, 2019 12:40 UTC
  • Nchi za Afrika zatakiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50

Tume ya Uchumi ya Afrika katika Umoja wa Mataifa (ECA) imetoa wito kwa nchi za Afrika kupunguza kwa nusu idadi ya watu wanaofarikia au kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani.

Taarifa iliyotolewa na ECA kwenye maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani ya Umoja wa Mataifa yenye kaulimbiu ya "Uongozi kwa ajili ya Usalama wa Barabarani", pia imesema, uongozi wenye nguvu ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika na nchi nyingine duniani zinadumisha usalama barabarani.

Kwa mujibu wa ECA, Lengo la 3.6 la Ajenda ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa linahitaji serikali zichukue hatua mpya kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

ECA inasema kuna mkakati wa kuchukua hatua madhubuti kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha au kujeruhiwa katika ajali za barabarani. Wataalamu wanatabiri kuwa watu milioni 1.9 wataendelea kupoteza maisha kila mwaka katika ajali za barabarani hadi mwaka 2020.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema ajali za barabarani ni mara tatu zaidi katika nchi masikini ikilinganishwa na nchi tajiri huku bara la Afrika likiwa na kiwango kikubwa zaidi cha ajali za barabarani duniani. Kwa mujibu wa uchaunguzi,  watu 26.6 kati ya 100,000 hupoteza maisha katika ajali za barabarani barani Afrika.

Ajali ya barabarani nchini Ethiopia

Aidha uchunguzi umebaini kuwa bara la Afrika lina asilimia 2 tu ya magari yaliyosajiliwa duniani katika hali ambayo asilimia 16 ya vifo vyote vinavyoripotiwa barabarani hutokea barani Afrika.

Sababu kuu ya ajali za barabarani Afrika imetajwa kuwa ni utengenezaji duni wa barabara, udhaifu katika utekelezwaji sheria, magari mabovu, watumizi wa barabara kukosa nidhamu na huduma duni za afya kwa wanaopata ajali barabarani.