Umoja wa Mataifa wataka kukabidhiwa madaraka Sudan kwa njia ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53405-umoja_wa_mataifa_wataka_kukabidhiwa_madaraka_sudan_kwa_njia_ya_amani
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande husika nchini Sudan kufanya juhudi za kudhamini ukabidhianaji madaraka kwa njia ya amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2019 21:49 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka kukabidhiwa madaraka Sudan kwa njia ya amani

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande husika nchini Sudan kufanya juhudi za kudhamini ukabidhianaji madaraka kwa njia ya amani.

Farhan Haq ametangaza kuwa, kuna haja ya hatua hiyo kufikiwa ili kutimiza matakwa ya wananchi wa Sudan kuhusiana na utekelezwaji wa demokrasia nchini humo baada ya kuondolewa madarakani Omar Hassan al-Bashir.

Farhan Haq amesema, Umoja wa Mataifa unazitajka pande husika nchini Sudan kuingia katika mazungumzo yatakayozishirikisha pande zote ili kutoa jibu kwa hitajio la hali ya sasa nchini humo.

Sudan kwa sasa inashuhudia mageuzi katika muundo wa kisiasa na kiutawala wa nchi hiyo kufuatia maandamano ya miezi kadhaa yaliyomuondoa madarakani Omar Hassan al-Bashir.

Viongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi nchini Sudan

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamekuwa wakilituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Waandamanaji hao wanasisitiza kwamba, Baraza la Mpito la Kijeshi linapaswa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia kama lilivyoahidi.

Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.

Baraza la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.