May 12, 2019 12:59 UTC
  • Wanajeshi 11 wa Nigeria wauawa na kundi la kigaidi la Boko Haram

Wanajeshi wasiopungua 11 wa Nigeria wameuawa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimeziambia duru za habari kwamba, shambulio hilo la Boko Haram limetekelezwa na wanamgambo hao katika mji wa Gajiganna ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, kufuatia kushadidi duru mpya ya mashambulio ya magaidi wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 katika eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao na kuishi kama wakimbizi katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria na kisha baadaye kupanua wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Hadi sasa mashambulio hayo yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini  na tano kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haramu, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo, na hivyo kukabiliwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Tags