Wananchi wa Sudan wazidi kushinikiza kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53435-wananchi_wa_sudan_wazidi_kushinikiza_kukabidhiwa_madaraka_kwa_utawala_wa_kiraia
Wapinzani nchini Sudan kwa mara nyingine tena wamesisitiza juu ya kutekelezwa takwa lao la kukabidhiwa madaraka ya nchi hiyo kwa utawala wa kiraia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2019 09:22 UTC
  • Wananchi wa Sudan wazidi kushinikiza kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia

Wapinzani nchini Sudan kwa mara nyingine tena wamesisitiza juu ya kutekelezwa takwa lao la kukabidhiwa madaraka ya nchi hiyo kwa utawala wa kiraia.

Wapinzani hao wametangaza kuwa, madhali Baraza la Mpito la Kijeshi halijakabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia maandamano na malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo yataendelea kushuhudiwa.

Taarifa ya wapinzani hao imeeleza kuwa, wananchi wa Sudan wamefanya maandamano na kuitisha migomo katika miji mbalimbali ya nchi hiyo na kutangaza wazi msimamo wao kuhusiana na suala zima la kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamekuwa wakilituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Viongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi Sudan

Waandamanaji hao wanasisitiza kwamba, Baraza la Mpito la Kijeshi linapaswa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia kama lilivyoahidi.

Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.