Homa ya Dengue yaongezeka Tanzania, mji wa Dar es Salaam unaongoza
Homa ya Dengue inaripotiwa kuongezeka katika miji mbalimbali ya Tanzania, huku jiji la Dar es Salaam likiripotiwa kuongoza kwa idadi ya watu wanaogua maradhi hayo.
Mganga Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mohamed Kambi amesema kuwa, kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, watu 1,901 wamepimwa na kuthibitika kuwa wana homa ya Dengue nchini humo.
Profesa Mohamed Kambi ameongeza kuwa, miongoni mwa wanaougua homa ya Dengue 1,809 kati yao wanatoka jijini Dar es Salaam, Tanga 89, ambapo mikoa ya Singida, Kilimanjaro na Pwani kila mmoja una mgonjwa mmoja.
Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania alisema hayo jana Alkhamisi wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa, wagonjwa wa mkoani Singida, Kilimanjaro na Pwani wote walitokea mkoa wa Dar es Salaam na waligunduliwa na ugonjwa huo baada ya kufika kwenye mikoa hiyo.
Aidha, hakuna vifo zaidi vilivyoripotiwa sasa mbali na viwili vilivyoripotiwa awali mwezi huu wa Mei huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari na endapo wataona dalili za ugonjwa huo, wawahi katika vituo vya afya kwa vipimo na matibabu.
Dalili za Homa ya Dengue ni pamoja na kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu ambapo dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati ya siku 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.
Mara ya mwisho Homa ya Dengue kuripotiwa kuibuka nchini Tanzaia ilikuwa mwaka 2014 ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.