Jeshi la Sudan kuanza tena mazungumzo na waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53580-jeshi_la_sudan_kuanza_tena_mazungumzo_na_waandamanaji
Baraza la Kijeshi linaloshikilia madaraka kwa muda nchini Sudan limetangaza kuwa mazungumzo na viongozi wa waandamanaji yataanza tena ili kutatua hitilafu zilizopo baina ya pande mbili kuhusu utawala wa mpito kabla ya kufanyika uchaguzi wa demokrasia nchini humo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 19, 2019 03:26 UTC
  • Jeshi la Sudan kuanza tena mazungumzo na waandamanaji

Baraza la Kijeshi linaloshikilia madaraka kwa muda nchini Sudan limetangaza kuwa mazungumzo na viongozi wa waandamanaji yataanza tena ili kutatua hitilafu zilizopo baina ya pande mbili kuhusu utawala wa mpito kabla ya kufanyika uchaguzi wa demokrasia nchini humo.

Katika taarifa, Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) limesema mazungumzo na Muungano kwa Ajili ya Uhuru na Mabadiliko yataanza tena leo Jumapili.  Pande mbili zimekuwa na mvutano kuhusu Mamlaka ya Mpito ambayo inapaswa kutawala nchi hiyo baada ya kutimuliwa madarakani dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al Bashir mwezi uliopita.

Jeshi linataka kuwa na viti vingi zaidi ya raia  katika baraza hilo ambalo litaiongoza nchi hiyo katika muda wa mpito. Hata hiyo  Muungano kwa Ajili ya Uhuru na Mabadiliko unasisitiza kuwa raia ndio wanaopaswa kuwa na viti vingi zaidi ya jeshi katika baraza hilo la mpito.

Mazungumzo baina ya pande mbili yalisitishwa na Baraza la Mpito la Kijeshi Alhamisi kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni kuzorota usalama katika mji mkuu, Khartoum ambapo waandamanaji waliweka vizingiti katika barabara muhimu. Karibu watu watano waliuawa wakati wanajeshi walipojaribu kuviondoa vizingiti hivyo.

Wananchi wa Sudan katika maandamano

Pande mbili zimeshafikia mapatano ya awali ikiwa ni pamoja na kuwepo kipindi cha mpito cha miaka mitatu na uundwaji wa bunge lenye wajumbe 300.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.