Rais Kiir wa Sudan Kusini ataka wapinzani kutekeleza mapatano ya amani
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amewataka viongozi wote wa upinzani kuchukua hatua za kivitendo katika kutekeleza makubaliano ya amani, ili kurejesha matumaini na matarajio ya wananchi.
Rais Kiir amesema, baada ya amani kupatikana, nchi hiyo changa zaidi duniani itatimiza maendeleo ya kasi kutokana na utajiri wake wa maliasili.
Amesema hayo katika uzinduzi wa jengo la wizara ya ulinzi ya Sudan Kusini, na kuongeza kuwa, kwa muda mrefu, maliasili za nchi hiyo zimepotea, ikiwemo rasilimali ya watu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Amesema kama nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya ndani, itaendelea kuwa na utulivu wa hivi sasa, itatimiza maendeleo makubwa ya miundombinu.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Nchi ya Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani.