May 26, 2019 07:37 UTC
  • Tishio la ugonjwa wa Ebola kuenea kote Afrika Mashariki

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC imetahadahrisha kuhusu tishio la ugonjwa hatari wa Ebola kuenea katika nchi za jumuiya hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye makao makuu yake mjini Arusha EAC imesema Ebola bado ni tishio kubwa kwa watu wa Afrika Mashariki, na kuonya kuhusu matokeo mabaya ya ugonjwa huo kwenye kilimo, utalii na maisha ya watu wa kanda hiyo.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Taarifa hiyo imetilia mkazo kuwa watu wanalazimika kujiandaa vizuri kuzuia ugonjwa huo usienee hadi nje ya mipaka ya DRC, ingawa hivi sasa hakuna wagonjwa wa Ebola walioripotiwa kuwepo kwenye nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa, endapo hali hiyo itaendelea kushuhudiwa, basi kuna hatari kubwa ya ugonjwa huo kusambaa hata katika nchi jirani.

Eneo la kuwatunza wanaougua ugonjwa wa Ebola

Taarifa ya WHO inaripotiwa siku chache baada ya kutolewa ripoti ya utafiti ulioonyesha kuwa, haiwezekani kudhibiti maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na yamkini maafa ya ugonjwa huo yakawa makubwa zaidi kuliko yale yaliyoshuhudiwa magharibi mwa Afrika mwaka 2013 na 2016.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kesi mpya 298 za Ebola zimethibitishwa nchini humo kati ya Aprili 15 na Mei tano mwaka huu.

Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

 

Tags