Wasudan waendeleza malalamiko ya umma
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53801-wasudan_waendeleza_malalamiko_ya_umma
Migomo ya umma imeanza tena nchini Sudan baada ya kushindwa mazungumzo baina ya wapinzani na Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2019 02:19 UTC
  • Wasudan waendeleza malalamiko ya umma

Migomo ya umma imeanza tena nchini Sudan baada ya kushindwa mazungumzo baina ya wapinzani na Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo.

Lengo la migomo hiyo iliyoitishwa na muungano wa Harakati ya Uhuru na Mabadiliko inayoundwa na makundi ya wapinzani, limetajwa kuwa ni kulishinikiza Baraza la Kijeshi likabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan umeshika mkondo mpana zaidi. Utendaji wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo katika kipindi cha baada ya kuondolewa madarakani Omar al Bashir umewakasirisha sana wapinzani wa kiongozi huyo wa zamani na makundi mbalimbali ya kisiasa. Wapinzani wanataka madaraka ya nchi yakabidhiwe mara moja kwa utawala wa kiraia, kuundwe serikali ya muda na kuitishwe uchaguzi utakaohakikisha kupokezana madaraka kwa njia ya kidemokrasia. Hata hivyo Baraza la Kijeshi linalodhibiti Sudan kwa sasa linasisitiza kuwa, hakuna udharura wa kukabidhi haraka madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Kuendelea kwa maandamano na migomo ya umma nchini Sudan kumelilazimisha Baraza la Kijeshi la Mpito liitishe mazungumzo juu ya mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo hususan masuala ya muundo wa serikali, muda wa serikali hiyo na wanachama wa baraza lake. Japokuwa katika duru ya kwanza ya mazungumzo hayo pande mbili zimefikia mwafaka kuhusu muda wa serikali ya mpito lakini bado kuna hitilafu kuhusu idadi ya wajumbe wa serikali ya mpito, idadi ya wanajeshi na raia katika serikali hiyo na jinsi ya kuainisha baraza la utawala. Kwa sasa mazungumzo hayo yamesimama na wapinzani wameitisha uasi wa kijamii. Wapinzani wanasema kuwa, Baraza la Mpito la Kijeshi halitaki utawala wa kisheria wala demokrasia. Vyama vya upinzani nchini Sudan vinaamini kuwa, sisitizo la Baraza la kijeshi la nchi hiyo la kuwepo kiongozi mwanajeshi wa baraza la utawala na suala la kuwepo idadi kubwa zaidi ya wanajeshi katika baraza hilo ni kikwazo katika njia ya kufanyika mageuzi na mabadiliko ya raia wa Sudan. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Jumuiya ya Wafanyakazi ya Sudan imelituhumu Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan kwa sasa kuwa linakwamisha jitihada za kuundwa baraza la utawala wa kiraia na imewataka Wasudan kufanya mgomo wa kijamii.

Wanajeshi wanaotawala Sudan kwa swasa

 

Wapinzani wanasisitiza kuwa, wataendeleza mgomo hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa. Wanasisitiza kuwa wana wasiwasi kuhusu mustakbali wa Sudan na kwamba idadi kubwa ya wajumbe wa Baraza la Kijeshi la serikali ya mpito inaundwa na mabaki ya maafisa wa serikali ya Omar al Bashir ambao hawawezi kufanya mabadiliko yanayosisitizwa na raia wa Sudan.  

Wasudan wanataka serikali ya kiraia

Makundi mengi ya wapinzani wa Sudan pia yana wasiwasi mkubwa kuhusiana na uingiliaji wa nchi za kigeni hususan Saudi Arabia na Imarati katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na mustakbali wake wa kisiasa.

Wasiwasi huo umeongezeka zaidi wakati wa safari iliyofanywa siku kadhaa zilizopita ya viongozi wa Baraza la Kijeshi la serikali ya mpito ya Sudan katika nchi za Saudia na Imarati. Vyama vya upinzani nchini Sudan vinaamini kuwa, baraza hilo linapewa misaada ya kifedha na kisilaha kutoka Saudi Arabia na Imarati na kwamba nchi hizo mbili zinapinga suala la kujitawala Sudan.

Azmi Bishara ambaye ni mhadhiri na mwanafikra maarufu wa Kiarabi anasema: Ushirikiano wa muungano wa nchi za Kiarabu zinazopinga demokrasia unaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati, haujali lolote isipokuwa udikteta wa kijeshi na unafanya jitihada za kufikia lengo hilo huko Sudan baada ya Misri na Libya.

Hata hivyo kuendelea kwa malalamiko ya wananchi huko Sudan kunaonesha kuwa, makundi ya upinzani yameazimia ipasavyo kuhakikisha kwamba, yanatimiza malengo ya mapinduzi ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha demokrasia na kufunga njia zote za satua na ushawishi wa madola ya kigeni nchini humo.