IGAD yasisitiza kuhusu usalama wa kipindi cha mpito Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53890-igad_yasisitiza_kuhusu_usalama_wa_kipindi_cha_mpito_sudan_kusini
Shirika la Kiserikali la Ustawi wa nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) limezihimiza pande zote za Sudan Kusini kushiriki kikamilifu katika mpango wa mpito wa usalama ili kusaidia utekelezwaji wa mapatano mapya ya amani kwa wakati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2019 03:48 UTC
  • IGAD yasisitiza kuhusu usalama wa kipindi cha mpito Sudan Kusini

Shirika la Kiserikali la Ustawi wa nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) limezihimiza pande zote za Sudan Kusini kushiriki kikamilifu katika mpango wa mpito wa usalama ili kusaidia utekelezwaji wa mapatano mapya ya amani kwa wakati.

Taarifa iliyotolewa na Mjumbe Maalum wa Shirika hilo nchini Sudan Kusini Bw. Ismael Wais imesema, utekelezaji wa Mapatano Mapya ya Utatuzi wa Mgogoro Sudan Kusini  (R-ARCSS) kwa kiasi kikubwa unategemea mipango ya usalama katika kipindi cha mpito.

Makubaliano mapya ya amani ya Sudan Kusini yanazitaka pande zote zinazopigana ziungane tena, lakini mchakato huo umeshindwa kukamilika kutokana na baadhi ya makundi kukataa kutangaza ukubwa wa vikosi vyao vya kivita.

Mapatano ya amani ya Sudan Kusini yalitiwa saini mwezi Septemba mwaka 2018, kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi, lakini yamekuwa yakikiukwa mara kwa mara.

Kinara wa upinzani Sudan Kusini Riek Machar

Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza tarehe 15 Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake wakati huo Riek Machar kwa madai kuwa alipanga njama ya kumpindua. Hadi sasa watu laki tatu na 85 elfu wameshauawa na mamilioni ya wengine kujeruhiwa na kuwa wakimbizi.

Sudan Kusini ilijitenga na ndugu zao wa Sudan mwaka 2011 na tangu wakati huo hadi sasa haijawahi kuwa na utulivu wa kudumu, bali imekuwa ikisumbuliwa na mizozo hii na ile.