Wapinzani Sudan wataka kuvunjwa Baraza la Kijeshi
Muungano wa Uhuru na Mabadiko unaoundwa na vyama vya upinzani nchini Sudan umetoa wito wa kuvunjwa Baraza la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Sudan dhidi ya waandamanaji ambayo yameua na kujeruhi makumi ya raia.
Taarifa ilyotolewa jana Jumatatu na muungano huo imetangaza mgomo wa kisiasa na uasi wa kijamii wa nchi nzima nchini Sudan. Muungano huo umetaka kufanyike jitihada za kukulipokonya madaraka Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo tangu baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir au kufanyika mgomo na maandamano ya nchi nzima.
Jumapili iliyopita jeshi la Sudan chini ya Baraza la Kijeshi linalotawala nchi liliwashambulia raia waliokuwa katika mgomo wa kuketi chini mbele ya makao makuu ya kamanda wa jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum. Ripoti zinasema watu wasiopungua 14 waliuawa na wengine 100 wamejeruuhiwa katika mashambulizi hayo.
Hali ya kisiasa nchini Sudan inaendelea kuyumbayumba tangu baada ya kupinduliwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir tarehe 11 Aprili mwaka huu.
Wananchi wa Sudan na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kiraia wanalitaka Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.