Jeshi Sudan latangaza uchaguzi mkuu; mauaji ya waandamanaji yazidi kulaaniwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53907-jeshi_sudan_latangaza_uchaguzi_mkuu_mauaji_ya_waandamanaji_yazidi_kulaaniwa
Jeshi nchini Sudan leo limetangaza kuvunja makubaliano yote ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia na badala yake limetangaza uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi tisa ijayo. Hayo yamekuja baada ya wanajeshi kushambulia waandamanaji na kuua raia 30 na kujeruhi mamia ya wengine jana Jumatatu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 04, 2019 02:22 UTC
  • Jeshi Sudan latangaza uchaguzi mkuu; mauaji ya waandamanaji yazidi kulaaniwa

Jeshi nchini Sudan leo limetangaza kuvunja makubaliano yote ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia na badala yake limetangaza uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi tisa ijayo. Hayo yamekuja baada ya wanajeshi kushambulia waandamanaji na kuua raia 30 na kujeruhi mamia ya wengine jana Jumatatu.

Baraza la Mpito la Kijeshi lililotwaa madaraka ya Sudan baada ya kumpindua rais Omar al Bashir mwezi Aprili mwaka huu kufuatia maandamano makubwa ya nchi nzima ya wananchi, limevunja makubaliano ya kuundwa serikali ya mpito ya miaka mitatu. Akizungumza kwa njia ya tarelevisheni, Jenerali Abdel Fattah al Burhan anayeongoza baraza hilo la kijeshi amesema kuwa uchaguzi mkuu utafanyika katika kipindi cha chini ya miezi tisa na utasimamiwa kieneo na kimataifa.

Itakumbukwa kuwa baada ya Umoja wa Mataifa kutoa taarifa na kuelezea kusikitishwa sana na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji nchini Sudan, Umoja wa Ulaya nao umetoa taarifa rasmi ya kupinga mauaji hayo na kulitaka jeshi la Sudan lisitumie nguvu kama hizo katika kukabiliana na wananchi wanaoandamana. 

Maandamano ya wananchi wa Sudan

 

Televisheni ya Rusia al Yaum imeunukuu Umoja wa Ulaya ukisema katika taarifa yake ya usiku wa kuamkia leo kwamba, umoja huo uko pamoja na familia za wahanga wananchi waliouawa na kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na wanajeshi na sambamba na kulaani mauaji hao umesema kuwa, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha mauaji na nguvu za kupita kiasi dhidi ya wananchi waliokusanyika kwa amani kutaka kutekelezewa matakwa yao. 

Taarifa ya Umoja wa Ulaya imesema kuwa, jukumu la Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ni kulinda usalama na kuheshimu utawala wa sheria hivyo linapaswa kufanya uvumilivu mkubwa katika kutekeleza wajibu huo. 

Umoja wa Ulaya vile vile umesema kuwa, matumizi yoyote ya mabavu yanaweza kuyatoa matukio ya Sudan katika mkondo wake wa kisiasa na kiusalama na kuutumbukiza kwenye mkwamo hatari. 

Kwa upande wake Kamati Kuu ya Madaktari nchini Sudan iliyoko karibu na waandamanaji imeandika katika ukurasa wake wa Facebook kwamba: "Idadi ya watu waliouawa katika mauaji ya leo (Jumatatu) ya umati wamefikia mashahidi tisa."

Jana pia Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa na kupinga vikali matumizi ya nguvu dhidi ya watu wanaoendesha maandamano ya amani ya kupigania haki zao za kikatiba huko Sudan.