CAR yawasaka waliotekeleza mauaji katika jimbo Paoua
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53943-car_yawasaka_waliotekeleza_mauaji_katika_jimbo_paoua
Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) inaendeleza jitihada za kuwasaka na kuwafikisha kizimbani waliotekeleza mauaji ya umati hivi karibuni katika jimbo la Paoua nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2019 22:04 UTC
  • CAR yawasaka waliotekeleza mauaji  katika jimbo Paoua

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) inaendeleza jitihada za kuwasaka na kuwafikisha kizimbani waliotekeleza mauaji ya umati hivi karibuni katika jimbo la Paoua nchini humo.

Kufuatia mauaji ya watu zaidi ya 30 yaliyofanywa na wanamgambo wa kundi linalojiita 3R kwenye jimbo la Paoua nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, serikali ya nchi hiyo imemtaka kiongozi wa kundi hicho ahakikishe wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria.

Tayari ujumbe wa serikali ukiambatana na wawakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya  nchi za Afrika ya Kati, ECCAS, na wawakilishi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA wameelekea Niem-Yelewa, mji ulio kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo ambao ni ngome ya kundi hilo la 3R.

Lengo la ziara hii kwenye jimbo la Bour ni kufahamu hasa sababu za mauaji hayo na kuwasilisha ombi maalum kwa kiongozi wa kundi hilo la 3R, Sidi Souleymane kuwafikisha wahusika wote wa mauaji hayo mbele ya sheria,  ingawa tayari ameshakabidhi watuhumiwa watatu.

Hatua hii  ya kuwasilisha ombi hilo kwake linazingatia kuwa kufuatia kutiwa saini  makubaliano mapya ya amani mwezi Februari mwaka huu kati ya serikali na makundi 14 ya wanamgambo, Souleymane alichaguliwa kuwa mshauri maalum wa kijeshi wa Waziri Mkuu, akihusika na ujumuishaji kwenye jeshi la serikali wanajeshi kutoka makundi mbalimbali ya wabeba silaha.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Henri Wanzet-Linguissara ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani CAR, anasema kuwa Souleymane yuko tayari kutoa ushirikiano kwa mkondo wa sheria. Kiongozi wa 3R amesisitiza kuwa waliotenda jinai hiyo walikuwa wahalifu na wala hawakuwa wanatekeleza amri za uongozi wa kundi hilo.

Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais  Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.