Umoja wa Mataifa: Tunaondoa askari wetu wa kusimamia amani nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53962-umoja_wa_mataifa_tunaondoa_askari_wetu_wa_kusimamia_amani_nchini_sudan
Kufuatia kuzorota hali ya usalama nchini Sudan, Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba utaondoa maafisa wake wasio wa kijeshi waliokuwa wakisimamia amani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2019 22:37 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Tunaondoa askari wetu wa kusimamia amani nchini Sudan

Kufuatia kuzorota hali ya usalama nchini Sudan, Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba utaondoa maafisa wake wasio wa kijeshi waliokuwa wakisimamia amani nchini humo.

Farhan Haq, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, pamoja na kwamba maafisa hao walikuwa tayari kubakia nchini Sudan kuitekeleza majukumu yao, lakini wataondolewa kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya. Hata hivyo Umoja wa Mataifa haukuweka wazi idadi kamili ya watumishi wake watakaosalia au kuondoka nchini Sudan au kwamba ni muda gani maafisa hao watarejea tena nchin humo. Shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Sudan zinajumuisha uimarishaji ushirikiano na shughuli za misaada ya kibinaadamu yakiwemo majukumu ya pamoja ya kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ambayo yamekuwa yakitekelezwa tangu mwaka 2007.

Farhan Haq, Msemaji wa Umoja wa Mataifa

Mgogoro wa nchi hiyo uliibuka Disemba mwaka jana baada ya wananchi kumiminika mabarabarani wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi ambapo kufuatia maandamano hayo, tarehe 11 Aprili mwaka huu jeshi la Sudan lilitangaza kumuondoa madarakani Rais Omar al-Bashir na kutwaa madaraka ya nchi hiyo. Baada ya hapo jeshi hilo liliunda Baraza la Kijeshi la Mpito ingawa wananchi wanalipinga na kulitaka liruhusu kuundwa serikali ya kiraia.