Wapinzani Sudan wakubali kwa masharti Ethiopia kuwa mpatanishi
Muungano wa upinzani nchini Sudan umeafiki kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed awe mpatanishi baina yao na Baraza la Mpito la Kijeshi ili kutatua mgogoro mkubwa wa kisiasa unaotokota nchini humo.
Kwa mujiibu wa taarifa, Jumuiya ya Wanataaluma Sudan (SPA) ambayo imekuwa mstari wa mbele kuongoza maandamano ya wananchi, siku ya Ijumaa ilitoa taarifa na kusema inaafiki upatanishi usio wa moja kwa moja wa Ethiopia na kusisitiza kuwa upatanishi wowote unapaswa kufanyika kwa lengo la kutekeleza mpango wa jeshi kuwakabidhi raia madaraka. Aidha jumuiya hiyo imetahadharisha kuhusu njama ya Baraza la Kijeshi la Mpito kutumia mamluki na wahuni kueneza fujo na kuwashambulia wapinzani katika maeneo mbali mbali ya mji mkuu Khartoum.
Abiy Ahmad Ali, Waziri Mkuu wa Ethiopia jana ijumaa alifika mjini Khartoum na kukutana na mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito Abdel Fattah Abdelrahman Burhan na ujumbe wa makundi ya wapinzani. Waziri Mkuu wa Ethiopia ametahadharisha kuhusu uingiliaji wa madola ya kigeni katika mambo ya ndani ya Sudan.
Wakati huo huo tovuti ya Middle East Eye imesema kwamba, Kiongozi wa Baraza la Kijeshi la Mpito huko Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan aliidhinishwa na Saudi Arabia na waitifaki wake kufanya mashambulizi dhidi ya raia waliokuwa wamekusanyika na kufanya mgomo mbele ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo Jumatatu iliyopita ambalo liliua zaidi ya raia mia moja.
Zaidi ya raia mia moja wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni kabisa ya jeshi la Sudan dhidi ya raia wanaoandamana kupinga utawala wa kijeshi.
Mgogoro wa Sudan uliibuka Disemba mwaka jana baada ya wananchi kumiminika mabarabarani wakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi ambapo kufuatia maandamano hayo, tarehe 11 Aprili mwaka huu jeshi la Sudan lilitangaza kumuondoa madarakani Rais Omar al-Bashir na kutwaa madaraka ya nchi hiyo. Baada ya hapo jeshi hilo liliunda Baraza la Kijeshi la Mpito ingawa wananchi wanalipinga na kulitaka liruhusu kuundwa serikali ya kiraia.