Umoja wa Mataifa walaani Jeshi la Sudan kwa kuua raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54079-umoja_wa_mataifa_walaani_jeshi_la_sudan_kwa_kuua_raia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelilaani jeshi la Sudan kwa kuwaua waandamanaji zaidi ya 100 katika machafuko yanayoendelea nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2019 09:14 UTC
  •  Umoja wa Mataifa walaani Jeshi la Sudan kwa kuua raia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelilaani jeshi la Sudan kwa kuwaua waandamanaji zaidi ya 100 katika machafuko yanayoendelea nchini humo.

Katika taarifa ambayo iliidhinishwa kwa kauli moja, wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wametoa wito kwa watawala wa kijeshi nchini Sudan kuacha kutumia mabavu dhidi ya raia sambamba na kusisitiza ulazima wa kulindwa haki za binadamu. Baraza hilo aidha limetoa wito kwa pande zote hasimu nchini Sudan kujitahidi kufikia muafaka ili kumaliza mgogoro wa sasa. Aidha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetangaza kuunga mjini jitihada za nchi za Afrika za kupatanisha baina ya viongozi wa waandamanaji na Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan ambalo linaunga mkono na Saudi Arabia.

Mnamo Juni 3 wanajeshi wa Sudan waliwapiga risasi na kuwaua raia zaidi ya 100 ambao walikuwa wamekusanyika na kufanya mgomo wa kukaa chini nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakitaka baraza la kijeshi liondoke madarakani. Wakati huo huo mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ametangaza kuwa takriban watoto 19 wameuuawa nchini Sudan na wengine 49 kujeruhiwa tangu Juni 3 mwaka huu amesema.

Maafisa wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan

Bi Henrietta Fore katika taarifa yale iliyotolewa Jumanne amesema “Ninatiwa hofu kubwa na athari za kuendelea vita na machafuko nchini Sudan kwa watoto na vijana hususan taarifa zinazoripotiwa za matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wanaoandamana kwa amani.”

Tokea Disemba mwaka 2018, wananchi wa Sudan walianzisha maandamano yao dhidi ya utawala wa kiimla wa Rais Omar al Bashir. Hatimaye mnamo Aprili 11 mwaka huu, walifanikiwa kumlazimisha al Bashir kuondoka madarakani baada ya kuitawala Sudan kwa takriban miaka 30. Baada ya al Bashir kutimuliwa, Baraza la Mpito la Kijeshi lilihodhi mamlaka ya uongozi na kuna ushahidi wa wazi kuwa, baraza hilo linaungwa mkono na Saudia pamoja na Imarati.