Jun 13, 2019 11:51 UTC
  • Mtu wa pili afariki dunia kwa Ebola Uganda, mijumuiko hadharani marufuku Kasese

Uganda imepiga marufuku mijumuiko hadharani katika Wilaya ya Kasese baada ya ugonjwa hatari wa Ebola kuibuka katika eneo hilo.

Msemaji wa Wizara ya Afya ya Uganda Emmanuel Ainebyona  amesema serikali imechukua hatua hiyo kuzuia ugonjwa huo ambao hadi sasa umepelekea watu wawili kufariki dunia katika eneo hilo wiki hii.

Siku ya Jumanne mvulana aliyekuwa na miaka mitano alifariki dunia Kasese baada ya kuugua Ebola kwa siku kadhaa. Mvulana huyo alikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na alifika Uganda kupata matibabu. Leo Alhamisi wakuu wa wizara ya afya nchini Uganda wamethibitisha kuaga dunia nyanya yake mtoto huyo ambaye pia amepoteza maisha kutokana na Ebola.

Wakati huo huo wataalamu kutoka Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Shirika la Afya Duniani WHO wamekutana wilayani Kasese, mashariki mwa Uganda kutathmini mlipuko wa Ebola.

Waziri wa Afya nchini Uganda Jane Ruth Aceng amesema, maofisa wa serikali na wataalamu wa afya wanakutana ili kubadilishana taarifa za jinsi ya kukabiliana na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Wakati huohuo, WHO imesema imepeleka dozi 3,500 za chanjo ya Ebola nchini Uganda baada ya mtu wa kwanza kuripotiwa kufariki dunia kwa ugonjwa huo nchini humo.

Chanjo ya Ebola

Habari nyingine zinasema, WHO imesema mlipuko wa Ebola nchini DRC umeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya na ustawi wa kiuchumi na kijamii kwa watu wa Afrika Mashariki. Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Tanzania Tigest Ketsela Mengestu ameitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea na mipango ya kitaifa na kikanda ya kuzuia kuenea Ebola.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kesi mpya 298 za Ebola zimethibitishwa nchini humo kati ya Aprili 15 na Mei tano mwaka huu.

WHO imesema hilo wakati huu inapoendelea kusaidia kupambana na maambukizi ya Ebola hasa mjini Beni, ambako watu zaidi ya 2,000 wameambukizwa na wengine 1,357 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti mwaka 2018.

 

Tags