Wapinzani nchini Sudan wataka kufanyike uchunguzi wa kimataifa wa mauaji ya waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54125-wapinzani_nchini_sudan_wataka_kufanyike_uchunguzi_wa_kimataifa_wa_mauaji_ya_waandamanaji
Muungano wa wapinzani nchini Sudan umesisitiza tena udharura wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu hujuma ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya waandamanaji ambayo imesema ni jinai dhidi ya taifa ambayo inahitajia uchunguzi usiopendelea upande wowote na wa wazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 14, 2019 23:52 UTC
  • Wapinzani nchini Sudan wataka kufanyike uchunguzi wa kimataifa wa mauaji ya waandamanaji

Muungano wa wapinzani nchini Sudan umesisitiza tena udharura wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu hujuma ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya waandamanaji ambayo imesema ni jinai dhidi ya taifa ambayo inahitajia uchunguzi usiopendelea upande wowote na wa wazi.

Taarifa iliyotolewa na muungano wa Uhuru na Mabadiliko unaojumuisha makundi ya upinzani ya Sudan imesema kuwa: Jitihada zinazofanywa na Baraza la Kijeshi la Mpito za kutaka kupunguza idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la hivi karibuni dhidi ya raia ni aibu na fedheha inayopaswa kulaaniwa. Taarifa hiyo imepinga madai ya watawala wa sasa wa Sudan ya kuwepo njama ya mapinduzi na kusisitiza kuwa, njama ya kutaka kuwahusisha wapinzani na jaribio la mapindizi ni sawa na juhudi za kutaka kufunika jua kwa kutumia kidole cha mkono. Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan umesisitiza kuwa, utaendelea kutumia njia za amani na nguvu ya wananchi kwa ajili ya kufanikisha mapinduzi ya raia na kutilia mkazo udharura wa kuwepo serikali ya mpito ya kiraia.

Baraza la Kijeshi la Sudan linakataa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Itakumbukwa kuwa mazungumzo baina ya Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan na muungano wa upinzani yalisimamishwa baada ya jeshi kushambulia mkusanyiko wa raia mbele ya makao makuu ya jeshi la kuua watu wasiopungua 100 hapo tarehe 3 Juni. Wapinzai nchini Sudan wanalitaka Baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Baraza hilo lilitwaa madaraka baada ya kuondolewa madaraka aliyekuwa rais wa Sudan, Omar al Bashir tarehe 11 Apili mwaka huu.