Homa ya Dengue yaua watu wanne nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54265-homa_ya_dengue_yaua_watu_wanne_nchini_tanzania
Serikali ya Tanzania leo Ijumaa imetoa kauli Bungeni kuhusu homa ya Dengue na kubainisha kwamba, tangu mwezi Januari hadi Juni mwaka huu 2019, watu wanne wamefariki dunia huku maelfu ya wengine wakiwa wameugua ugonjwa huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2019 09:55 UTC
  • Homa ya Dengue yaua watu wanne nchini Tanzania

Serikali ya Tanzania leo Ijumaa imetoa kauli Bungeni kuhusu homa ya Dengue na kubainisha kwamba, tangu mwezi Januari hadi Juni mwaka huu 2019, watu wanne wamefariki dunia huku maelfu ya wengine wakiwa wameugua ugonjwa huo.

Kwa  mujibu wa Waziri wa Afya nchini humo, Ummy Mwalimu, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, watu wanne wameaga dunia huku wengine 4,320 wakithibitika kuwa wana homa hiyo hatari.

Amesema kati ya vifo vinne vilivyoripotiwa, vitatu vimetokea katika mji mkuu Dar es Salaam. Kifo cha nne kimeripotiwa mkoani Dodoma, mbali na wagonjwa watatu.

Waziri Ummy Mwalimu ameagiza kufanyika vipimo bila malipo katika hospitali, zahanati na vituo vyote vya afya vya umma nchini humo.

Vifo viwili viliripotiwa mapema mwezi uliopita wa Mei kutokana na ugonjwa huo hatari, huku serikali ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari na endapo wataona dalili za ugonjwa huo, wawahi katika vituo vya afya kwa vipimo na matibabu.

Mbu wanaosambaza homa ya Dengue

Mripuko mpya wa homa ya Dengue uliripotiwa nchini Tanzania Aprili mwaka huu katika ukanda wa pwani, ambapo taarifa za awali zilisema watu zaidi ya 300 wameambukizwa.

Dalili za Homa ya Dengue ni pamoja na  kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu ambapo dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati ya siku 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya Dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.