Majenerali wa Kijeshi Sudan wadai hawafuati sera za al Bashir
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54466-majenerali_wa_kijeshi_sudan_wadai_hawafuati_sera_za_al_bashir
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Sudan amedai kuwa baraza hilo si muendelezo wa serikali ya Field Marshal Omar al Bashir aliyepinduliwa na jeshi mwezi Aprili mwaka huu baada ya kushadidi maandamano ya wananchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2019 11:07 UTC
  • Majenerali wa Kijeshi Sudan wadai hawafuati sera za al Bashir

Naibu wa Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Sudan amedai kuwa baraza hilo si muendelezo wa serikali ya Field Marshal Omar al Bashir aliyepinduliwa na jeshi mwezi Aprili mwaka huu baada ya kushadidi maandamano ya wananchi.

Televisheni ya al Manar imemnukuu Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu kwa jina la Hemedti akidai kuwa, kazi ya wanajeshi wa Sudan ni kulinda usalama wa raia na si kupambana nao mitaani.

Hemedti amezungumzia pia kupewa fursa mafisadi na wahalifu kujirekebisha na kuongeza kwamba, baraza la kijeshi la Sudan linataka kuundwe serikali ya kiraia itakayoongozwa na watu huru na wanaostahiki kuwa viongozi.

Maandamano na upinzani wa wananchi unaendelea Sudan

 

Jenerali huyo wa kijeshi wa Sudan ambaye aliwahi pia kuwa mkuu wa wanamgambo wa Janjawid wanaotuhumiwa kufanya jinai za kivita huko Darfur, magharibi mwa Sudan amedai kuwa baraza la kijeshi la nchi hiyo linafanya juhudi za kuandaa mazingira mazuri ya maisha kwa Wasudan wa matabaka yote na kuandaa nafasi za kazi katika taasisi za serikali, za kijeshi na za kijamii.

Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Field Marshal Omar al Bashir. Hata hivyo wananchi wamekasirishwa na hatua hiyo wakisema ni ujanja tu wa jeshi la Sudan wa kuhakikisha linapindua mapinduzi ya wananchi na kuendelea kuhodhi madaraka ya nchi.

Wapinzani wanasema kuwa uamuzi wa Baraza la Kijeshi la Sudan wa kutumia nguvu kukandamiza wananchi una uhusiano wa moja kwa moja na ziara ya maafisa wa ngazi za juu wa baraza hilo katika nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri.