Wanajeshi wakandamiza maandamano ya wananchi Sudan; watu saba wauawa
Watu wasiopungua saba wanaripotiwa kuuawa nchini Sudan baada ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kutumia mkono wa chuma kuyakandamiza maandamano ya wananchi ya kutaka utawala wa kiraia.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, maandamano makubwa ya jana ya wananchi wa Sudan katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum yaligeuka kuwa umwagaji damu baada ya vikosi vya usalama kuwavamia waandamanaji na kuwafyatulia risasi.
Wananchi hao walikuwa wakishiriki katika maandamano ya kutoa wito kwa Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo kukabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
Duru za hospitali zinasema kuwa, watu karibu mia mbili wamejeruhiwa katika ukandamizaji huo wa vikosi vya usalama vya Sudan.
Mauaji hayo yametokea masaa machache tu baada ya Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan kutangaza kuwa, liko tayari kuanza mazungumzo na wapinzani wake na kudai kwamba, utatuzi wowote wa mgogoro huo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa usimamizi wa Umoja wa Afrika.
Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Omar Hassan al-Bashir. Hata hivyo wananchi wamekasirishwa na hatua hiyo wakisema ni ujanja tu wa jeshi la Sudan wa kuhakikisha linapindua mapinduzi ya wananchi na kuendelea kuhodhi madaraka ya nchi.
Wapinzani wanasema kuwa uamuzi wa Baraza la Kijeshi la Sudan wa kutumia nguvu kukandamiza wananchi una uhusiano wa moja kwa moja na safari za maafisa wa ngazi za juu wa baraza hilo katika nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri.