AU: Makubaliano kati ya jeshi na waandamanaji Sudan yanakaribia kufikiwa
Mjumbe wa Umoja wa Afrika anayeongoza timu ya upatanishi katika mgogoro wa Sudan amesema pande hasimu nchini humo zinatazamiwa kufikia makubaliano 'hivi karibuni'.
Mohamed Hacen El Lebatt alisema hayo jana Jumanne mjini Khartoum katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mahmud Dirir, mpatanishi wa mgogoro wa Sudan kutoka Ethiopia, ambapo amesisitiza kuwa majadiliano yanaendelea ili kuhakikisha kuwa pande zote zinakubaliana katika masuala machache wanayotofautiana juu yake.
Naye Mahmud Dirir, mpatanishi wa mgogoro wa Sudan kutoka Ethiopia amelitaka Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan na viongozi wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko unaoongoza maandamano ya wananchi kukutana leo Jumatano katika mazungumzo ya ana kwa ana ili kutatua hitilafu zilizopo.
Pande mbili hizo zimekuwa zikitofautiana kuhusu idadi ya shakhsia watakaoongoza Baraza la Mpito na muda wa kipindi cha mpito kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.
Jumapili iliyopita, Baraza la Kijeshi la Mpito lilikabili kwa mkono wa chuma maandamano ya wananchi, ambapo watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa. Jamal Jumma Adam, msemaji wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha (RSF) amesema askari mmoja aliuawa na wengine 29 wakajeruhiwa pia katika ghasia hizo za Jumapili.
Itakumbukwa kuwa, katika maandamano ya mwezi Mei, zaidi ya raia 118 waliuawa na vikosi vya usalama mbele ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.