Sudan kushuhudia maridhiano jumuishi ya kitaifa katika kipindi cha mpito
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54587-sudan_kushuhudia_maridhiano_jumuishi_ya_kitaifa_katika_kipindi_cha_mpito
Muungano wa Uhuru na Mageuzi nchini Sudan umetangaza kuwa, nchi hiyo itashuhudia kuanza maridhiano jumuishi ya kitaifa katika kipindi cha utawala wa mpito.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2019 03:47 UTC
  • Sudan kushuhudia maridhiano jumuishi ya kitaifa katika kipindi cha mpito

Muungano wa Uhuru na Mageuzi nchini Sudan umetangaza kuwa, nchi hiyo itashuhudia kuanza maridhiano jumuishi ya kitaifa katika kipindi cha utawala wa mpito.

Taarifa ya muungano huo ambao kwa miezi kadhaa umeongoza maandamano ya kulishinikiza Baraza la Kijeshi la Mpito likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia umetangaza leo kuwa, Sudan itashuhudia kuanza maridhiano makubwa yya kitaifa katika kipindi cha utawala wa mpito.

Tayari wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mageuzi wameafikiana juu ya suala la kugawana madaraka katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu kuelekea katika uchaguzi. 

Mwafaka huo ni matunda ya mazungumzo ya moja kwa moja ya siku mbili mjini Khartoum, juu ya kipindi cha mpito na idadi ya wawakilishi wa kila upande katika baraza la uongozi la kipindi hicho cha mpito.

Moja ya vikao vya mazungumzo kati ya Baraza la Kijeshi la Mpito na viongozi wa Muungano wa Uhuru na Mageuzi nchini Sudan

Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Omar Hassan al-Bashir. Hata hivyo wananchi wamekasirishwa na hatua hiyo wakisema ni ujanja tu wa jeshi la Sudan wa kuhakikisha linapindua mapinduzi ya wananchi na kuendelea kuhodhi madaraka ya nchi.

Wapinzani wanasema kuwa, uamuzi wa Baraza la Kijeshi la Sudan wa kutumia nguvu kukandamiza wananchi una uhusiano wa moja kwa moja na safari za maafisa wa ngazi za juu wa baraza hilo katika nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri.