Al Ghannouchi kushiriki uchaguzi wa bunge Tunisia
Kiongozi wa chama cha Kiislamu cha An Nahdhah cha nchini Tunisia ametangaza rasmi kuwa atashiriki katika uchaguzi ujao wa bunge wa nchi hiyo.
Imed al Khmiri msemaji wa chama cha An Nahdhah amebainisha kuwa chama hicho kimemtangaza rasmi Rashid al Ghannouchi kuwa atagombea katika uchaguzi wa bunge la nchi hiyo uliopangwa kufanyika mwezi Otoba mwaka huu. Vyombo vya habari vimearifu kuwa Al Ghannouchi anafanya jitihada katika marhala ijayo awe Waziri Mkuu au Spika wa Bunge iwapo chama chake kitashinda uchaguzi. Rashid Ghannouchi hajawahi kugombea rasmi nafasi yoyote katika vyombo vya utendaji au utungaji sheria nchini Tunisia. Kiongozi huyo wa chama cha Kiislamu cha An Nahdhah anafahamika kama mwanasiasa anayepinga mfumo wa kisiasa wa zamani wa Tunisia.
Kiongozi huyo wa chama cha An Nahdhah chenye misimamo ya wastani ambaye aliwahi kuwa uhamishoni London Uingereza kwa muda usiopungua miongo miwili wakati wa utawala wa Zainul Abidin bin Ali Rais wa zamani wa Tunisia; alirejea katika maisha ya kisiasa baada ya mapinduzi ya mwaka 2011 nchini kwake. Tangu wakati huo Rashid Ghannouchi hajawahi kugombea wadhifa wowote serikalini.