Aug 13, 2019 07:09 UTC
  • SADC kuisaidia DRC kukabiliana ugonjwa wa Ebola

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC zimeunganisha nguvu kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Mkurugenzi wa sekretariet ya siasa, ulinzi na usalama ya SADC Jorge Cardoso amesema, mawaziri wa afya kutoka nchi 16 wanachama wa Jumuiya hiyo walikutana hivi karibuni kujadili njia nzuri za kuisaidia DRC kupambana na Ebola.

Akizungumza akiwa mjini Dar es Salaam, Cardoso amesema viongozi wa SADC watakaokutana mjini humo kati ya Agosti 17-18 watajadili kwa kina kadhia ya vita dhidi ya Ebola.

Huku hayo yakijiri taarifa ya Shirika la Afya Duniani imeeleza kuwa zoezi la utoaji chanjo linaloendelea sasa huko DRC limefikia kiwango cha asilimia 98. Aidha hakuna kesi mpya za maambukizo ya Ebola zilizothibitishwa huko Goma tangu WHO iwasilishe ripoti yake ya mwisho tarehe pili mwezi huu.

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Dunaini (WHO) hivi karibuni lilitangaza kuwa kwa wastani watu 86 wanaambukizwa ugonjwa wa Ebola kila wiki nchini Jamhuri ya Kdemokrasia ya Kongo,  katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti, jumla ya visa 2,781 vimeripotiwa tangu kulipuka kwa ugonjwa huo Kivu Kaskazini mwezi Agosti mwaka jana na kati ya visa hivyo, wagonjwa 1,866 waliothibitishwa kuambukizwa wamefariki dunia.

Tags