UN: Mvua na mafuriko yameua watu 78 nchini Sudan
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema kuwa mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini Sudan yameua makumi ya watu.
Mary Keller, afisa wa ngazi za juu wa OCHA ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, akthari ya vifo hivyo vimesababishwa na kuporomoka kwa mapaa ya nyumba huku wengine wakiaga dunia kwa kupigwa na umeme.
Amebainisha kuwa, majimbo 16 kati ya 18 kote Sudan yamekumbwa na mafuriko hayo na kwamba nyumba 41,000 zimeharibiwa na janga hilo la kimaumbile.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA amesisitiza kuwa, kuna haja ya kuchukua hatua za kuzuia kuenea magonjwa yanayotokana na maji machafu katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko nchini Sudan, huku akionya kuwa yumkini idadi ya waathirika wa mafuriko hayo ikaongezeka.
Mwezi uliopita wa Agosti, serikali ya Sudan iliripoti kuwa, zaidi ya mifugo 3,600 imesombwa na maji huku mafuriko hayo yakiharibu pia mashamba ya kilimo.