Rais wa Kenya aidhinisha sheria dhidi ya pufya
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo ameidhinisha sheria zitakatambua pufya au doping kuwa kosa la jinai.
Baada ya kukosa kutimiza makataa ya kupitisha sheria hiyo Februari 11, 2016 na tena Aprili 5, 2016 kutoka kwa Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya Duniani (WADA), Kenya sasa imekukubali sheria hizo kabla ya makataa ya tatu iliyopangwa kukamilika Mei 2, 2016. Iwapo Kenya haingepitisha sheria hizo basi huwenda ingewekewa vikwazo na yamkini ingepigwa marufuku kushiriki katika Mashindano ya Olimpiki ya Rio de Janeiro hapo mwaka huu.
Baadhi ya adhabu katika sheria hii mpya ni wanariadha wanaokataa kupimwa, wanaopatikana na uhalifu wa dawa hizo haramu, wanadanganya shirika la kukabiliana na uovu huu ama kusumbua kazi yake kufungwa jela mwaka mmoja ama faini ya Sh100, 000 au kutumikia adhabu hizo zote.
Watu watakaopatikana wakisafirisha, kuweka ama kuwapa wanaspoti dawa zilizopigwa marufuku na WADA watatozwa faini ya Sh 3 milioni ama kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani ama adhabu hizi zote.
Wahudumu wa afya au madaktari wanaotoa tiba za asili pia watakamatwa na mkono mrefu wa sheria na kufungwa jela miaka mitatu au kutozwa faini ya Sh 3 milioni au kutumikia adhabu hizi zote.
Shughuli ya kutia saini sheria hiyo imefanyika katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi na kushuhudiwa na wanaspoti watajika wakiongozwa na Waziri wa Michezo, Dkt Hassan Wario.
Rais Kenyatta amesema kuharamishwa uovu huo ni mwanzo tu wa vita dhidi ya matumizi ya pufya na kwamba serikali inanuia kuendeleza juhudi za kuhakikisha kwamba udanganyifu na ufisadi katika spoti na riadha unamalizwa.
Vilevile amewataka Wakenya kukoma kutumia njia ya mkato na badala yake kushinda kwa njia ya haki akiamini wanao uwezo huo.
Rais Kenyatta ana matumaini makubwa kuwa WADA itaona kupitishwa kwa sheria hizi kama njia moja ya Kenya kujitolea kwa dhati kufikia viwango vya juu kabisa vya kimataifa. Zaidi ya Wakenya 40 walipatikana kuwa wahalifu wa dawa za kusisimua misuli kati ya mwaka 2012 na 2015.