Wanajeshi 3 waaga dunia katika ajali ya helikopta CAR
Askari watatu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (Minusca) wamepoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea jana Ijumaa.
Jeshi la Senegal limetangaza kuwa, askari hao walioaga dunia katika ajali hiyo ni raia wa nchi hiyo. Habari zaidi zinasema kuwa, helikopta iliyokuwa imewabeba askari hao ilianguka katika mji wa Bouar, wakati ikitoka katika operesheni ya kiusalama na kwamba mtu mmoja amejeruhiwa vibaya katika ajali hiyo.
Imeelezwa kuwa, helikopta hiyo ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ilianguka wakati ikikaribia kutua, kutokana na ukungu mzito uliokuwa umetanda angani.
Kazi ya askari wapatao elfu 11 na 650, pamoja na polisi 2000 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ilitakiwa kufikia tamati katikati ya mwezi Novemba mwaka jana, lakini wakaongezewa muda kufuatia ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé.
Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.