Oct 28, 2019 12:28 UTC
  • Amnesty, HRW zaijia juu serikali ya Tanzania kwa kukiuka haki za binadamu

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yameituhumu serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kuwa inakiuka haki za binadamu.

Ripoti mbili tofauti zilizotolewa na mashirika hayo leo Jumatatu zimedai kuwa, tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, Tanzania imekuwa ikitekeleza sheria ambazo zinabinya uhuru wa vyombo vya habari sambamba na kubana harakati za vyama vya siasa na mashirika ya kiraia.

Ripoti hizo zimesema utawala wa Magufuli umeshadidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani, na sera za serikali hiyo zimeondoa mlingano na usawa kwa vyama vinavyotaka kuchuana na chama tawala.

 Jehanne Henry, Mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Afrika Mashariki amesema, "Katika hali ambayo msimu wa uchaguzi umekaribia, lakini wananchi hawahisi kama wako huru kujieleza na kutoa maoni yao kwa uhuru."

Kamatakamata ya polisi Tanzania

Naye Roland Ebole, mtafiti wa Amnesty International nchini Tanzania amesema, "Tunashuhudia mwenendo hatari wa ukandamizaji nchini Tanzania. Mamlaka imewanyima wananchi haki yao ya kupata taarifa, na wamekuwa wakilazimika kupokea tu taarifa  zinazotajwa kuwa 'sahihi' na serikali."

Ripoti hizo za mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch zimeitaka serikali ya Dar es Salaam ifutilie mbali mashitaka yanayowakabili waandishi wa habari na wanaharakati wa kisiasa nchini humo, ambao walikamatwa wakitekeleza uhuru wao wa kujieleza na kukusanyika.

Tags