Njama za Saudia na Imarati za kusambaratisha mapinduzi ya Sudan zalalamikiwa
Chama cha Kikomonisti cha Sudan kimezituhumu Saudi Arabia na Imarati kwamba, zinafanya njama za kusambaratisha mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.
Muhammad Mukhtar al-Khatib, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Sudan na mmoja wa wajumbe wa Muungano wa Uhuru na Ukombozi wa Sudan sambamba na kuzituhumu Imarati na Saudia kwamba, zimekuwa zikifanya njama za kuvuruga mapinduzi hayo ya wananchi, ametoa wito wa kuondoka vikosi vya Khartoum katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen.
Mukhtar al-Khatib amekosoa vikali hatua ya Saudi Arabia na Imarati ya kuwasiliana na baadhi ya makundi ya kisiasa na viongozi muhimu wa upinzani zikifanya njama za kuyaondoa mapinduzi ya Sudan katika mkondo wake wa asili.
Katibu mkuu huyo wa The Sudanese Communist Party amesema kuwa, baadhi ya mataifa kutokana na kuhofia kutokea katika nchi hizo mapinduzi kama ya Sudan, viongozi wao wamekuwa wakifanya njama za kuyaondoa katika mkondo wake mapinduzi ya Sudan.
Kadhalika mwanasiasa huyo amesema kuwa, chama chake kinapinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan.
Omar Hassan al-Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka huu kufuatia maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa ya wananchi. Maandamano hayo yalichochewa na hali mbaya ya uchumi, ufisadi mkubwa na utumiaji mbaya wa madaraka wa al-Bashir.