Sudan yazindua satalaiti yake ya kwanza iliyounda kwa ushirikiano na China
Sudan imezindua kwa kurusha angani satalaiti yake ya kwanza itakayoshughulika na utafiti wa kijeshi, kiuchumi na wa tekonolojia ya anga za mbali. Akizungumza katika kikao na maafisa waandamizi wa usalama, mkuu wa Baraza Kuu la Utawala la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametangaza kuwa, satalaiti hiyo imetengezwa kwa ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa China.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imesema, satalaiti hiyo imeundwa kwa lengo la kuendeleza utafiti katika teknolojia ya anga za mbali, kukusanya taarifa na vile vile kugundua maliasili kwa ajili ya mahitaji ya kijeshi ya nchi.
Shirika rasmi la habari la China Xinhua limeripoti kuwa, Satalaiti ya Sudan ya Kukusanya Taarifa kutokea mbali iitwayo SRSS-1 ilirushwa kuelekea angani siku ya Jumapili katika mkoa wa Shanxi, kaskazini mwa China.
Msemaji wa baraza la utawala la Sudan Mohamed al-Faki Suleiman amesema, baada ya muda wa miezi michache, satalaiti hiyo itakuwa inaongozwa kutokea Sudan. Ameongeza kuwa China imerusha satalaiti hiyo kama mshirika katika mradi wa uundaji wake.
Sudan, ambayo inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi imekuwa ikiendesha mradi wa kitaifa wa teknolojia ya anga za mbali kwa muda wa miongo kadhaa sasa.
Mnamo mwaka 2013 , serikali ya Sudan ya wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na Omar al-Bashir ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Anga za Juu na Anga za Mbali (ISRA), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza teknolojia za anga za mbali.../