Sudan inahitaji dola bilioni 5 kusaidia bajeti ya nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57143-sudan_inahitaji_dola_bilioni_5_kusaidia_bajeti_ya_nchi
Waziri wa Fedha wa Sudan amesema kuwa nchi hiyo inahitaji kiasi cha dola zipatazo bilioni 5 ili kusaidia bajeti ya nchi na hivyo kuzuia kuporomoka uchumi wa nchi na kusaidia kutekelezwa marekebisho mbalimbali baada ya kupinduliwa mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Nov 08, 2019 23:44 UTC
  • Sudan inahitaji dola bilioni 5 kusaidia bajeti ya nchi

Waziri wa Fedha wa Sudan amesema kuwa nchi hiyo inahitaji kiasi cha dola zipatazo bilioni 5 ili kusaidia bajeti ya nchi na hivyo kuzuia kuporomoka uchumi wa nchi na kusaidia kutekelezwa marekebisho mbalimbali baada ya kupinduliwa mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Ibrahim Elbadawi Waziri wa Fedha wa Sudan aliyeteuliwa katika serikali ya mpito ya nchi hiyo iliyoundwa mwezi Agosti mwaka huu amesema kuwa, nchi hiyo ambayo iko katika mgogoro tangu baada ya kupoteza aghalabu ya utajiri wake wa mafuta kufuatia kujitenga na Sudan Kusini mwaka 2011,  hivi sasa ina akiba ya fedha za kigeni za kugharamia bidhaa kutoka nchi za nje kwa wiki kadhaa tu.

Amesema Sudan imepata msaada wa mafuta na nafaka kutoka nje, hata hivyo asilimia karibu 65 ya jamii ya watu milioni 44 wa nchi hiyo wanaishi katika hali ya umaskini. Amesema kwa msingi huo Sudan inahitaji pesa za maendeleo kiasi cha dola bilioni 2 na ahadi ya dola bilioni mbili kutoka fedha za maendeleo za nchi za kiarabu. 

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Fedha wa Sudan ikiwa ni mara yake ya kwanza akiweka wazi mipango ya marekebisho tangu ashike hatamu za kuongoza wizara hiyo mwezi Agosti mwaka huu. Ameongeza kuwa, mishahara ya wafanyakazi wa serikali pia itahitajia kuongezwa. 

Itakumbukwa kuwa miezi kadhaa ya karibuni Sudan ilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wakilalamikia kupanda bei ya petroli na mkate; maandamano ambayo yaliibua upinzani dhidi ya Rais al Bashir na hatimaye jeshi la nchi hiyo mwezi Aprili mwaka huu likamuondoa madarakani kiongozi huyo aliyehudumu kwa muda mrefu.  

Omar Hassan al Bashir, Rais wa Sudan aliyepinduliwa