Sudan yapasisha sheria ya kufutiliwa mbali utawala na chama cha al Bashir
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57566-sudan_yapasisha_sheria_ya_kufutiliwa_mbali_utawala_na_chama_cha_al_bashir
Serikali ya mpito ya Sudan imepasisha rasmi sheria ya kuvunjilia mbali utawala wa rais aliyeondolewa madarakani wa nchi hiyo, Omar al bashir na chama chake.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 29, 2019 03:24 UTC
  • Al Bashir akiwa kizimbani
    Al Bashir akiwa kizimbani

Serikali ya mpito ya Sudan imepasisha rasmi sheria ya kuvunjilia mbali utawala wa rais aliyeondolewa madarakani wa nchi hiyo, Omar al bashir na chama chake.

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok amesema kuwa, sheria ya kuvunjilia mbali utawala wa Omar al Bashir ilipasishwa jana katika kikao cha Baraza la Utawala wa Mpito na baraza la mawaziri. Hamdok amesema hatua hiyo haikuchukuliwa kwa lengo la kulipiza kisasi bali ni kwa ajili ya kulinda heshima ya taifa baada ya kukanyagwa na madikteta.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan amesema sheria hiyo pia imepasishwa kwa shabaha ya kurejesha uadilifu na kulinda matunda ya wananchi wa Sudan na vilevile kurejesha mali ya wananchi iliyoporwa. 

Abdallah Hamdok

Wakati huo huo Wajdi Saleh ambaye ni miongoni mwa vinara wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan amesema kuwa, sheria ya kufutiliwa mbali utawala Omar al Bashir inajumuisha kuvunjwa chama chake cha Kongresi ya Taifa, taasisi zote za chama hicho na nembo zote za serikali iliyoondolewa madarakani ya al Bashir.

Omar Al Bashir alipinduliwa na jeshi mwezi Aprili mwaka huu kufuatia maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi wa Sudan dhidi ya utawala wake wa muda mrefu.