Wasudan wataka askari wa nchi hiyo walioko Yemen warejeshwe nchini
Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi wa Sudan tawi la kaskazini ametoa wito wa kurejeshwa nyumbani wanajeshi wa Sudan wanaopigana kwa niaba ya Sudi Arabia nchini Yemen.
Yasir Arman amesema wanajeshi wa Sudan wanaoshiriki katika vita vinavyoongozwa na Sauudi Arabia huko Yemen wanapaswa kurejeshwa nyumbani na kuongeza kuwa, uamuzi wa kupelekwa wanajeshi hao katika vita vya Yamen uliochukuliwa na rais aliyeondolewa madarakani wa Sudan, Omar al Bashir na kwamba Wasudan hawa uhasama na taifa la Yemen.
Arman ametoa wito wa kuundwa upya jeshi la Sudan na kusema: Omar al Bashir alitoa pigo kubwa zaidi kwa jeshi la Sudan na kulitumbukiza katika vita vya muda mrefu.
Makundi mbalimbali ya kisiasa ya Sudan yamekuwa yakitoa wito wa kurejeshwa nyumbani wanajeshi wa Sudan wanaoshiriki katika muungano wa vita wa Saudi Arabia dhidi ya taifa la Yemen kwa karibu miaka 5 sasa.
Upinzani wa Wasudan dhidi ya kutumwa awanajeshi wa Sudan katika vita vya Yemen ulianza katika kipindi cha utawala wa al Bashir na umeshika kasi zaidi baada ya kiongozi huyo kuondolewa madarakani.
Al Bashr anashikiliwa katika jela moja nchini Sudan kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka, kula rushwa, ufisadi na kadhalika.
Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Sudan Taj Al Sir Ali Al Habr amesema ameunda kamati kuchunguza mapinduzi ya kijeshi ya Juni 30 1988 ambayo yaliongozwa na Bashir.
Matokeo ya uchunguzi huo yatakuwa msingi wa kuwashtaki wale wote waliohusika katika kukiuka mfumo wa kikatiba nchini Sudan wakati huo.
Iwapo watapatikana na hatia, waliohusika katika mapinduzi hayo ya kijeshi wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela au kunyongwa.