Mkasa wa moto katika kiwanda cha vigae waua 23 Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57667-mkasa_wa_moto_katika_kiwanda_cha_vigae_waua_23_sudan
Kwa akali watu 23 wamepoteza maisha huku makumi ya wengine wakijeruhiwa kutokana na ajali ya moto iliyokikumba kiwanda kimoja cha kutengeneza vigae katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2019 03:45 UTC
  • Mkasa wa moto katika kiwanda cha vigae waua 23 Sudan

Kwa akali watu 23 wamepoteza maisha huku makumi ya wengine wakijeruhiwa kutokana na ajali ya moto iliyokikumba kiwanda kimoja cha kutengeneza vigae katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Afisa wa polisi kwa jina Mohammed al-Khatem Hassan amewaambia waandishi wa habari mjini Khartoum kuwa, moto huo umesababishwa na mlipuko wa lori la gesi lililokuwa likipakua mizigo katika kiwanda hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Mawaziri la Sudan, majeruhi zaidi ya 130 wanapatiwa matibabu katika hospitali zilizo karibu na eneo la tukio.

Duru za hospitali zinaarifu kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na majereha mabaya waliyoyapata manusura wa mkasa huo wa jana Jumanne.

Mikasa ya moto imekithiri katika miezi ya hivi karibuni nchini Sudan

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Said Mohammed al-Hassan ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, "Tulihisi mtetemeko mkubwa na kuelekea mbio kwenye eneo la tukio kushuhudia kilichokuwa kinajiri. Tulipigwa na butwaa tulipoona wingu zito la moto huku kila mmoja akikimbia huku na kule kunusuru maisha yake."

Sudan imekuwa ikikabiliwa na majanga ya moto katika miezi ya hivi karibuni, ambapo mapema mwaka huu, sehemu ya jengo la Ikulu ya Rais mjini Khartoum iliteketezwa kwa moto katika tukio ambalo liliwashangaza wengi.