Jan 01, 2020 07:52 UTC
  • Khalifa Haftar anajaribu kueneza wigo wa kimataifa wa mgogoro wa Libya

Baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani na hivi sasa kuna serikali mbili hasimu, moja ya mashariki na nyingine ya magharibi mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya pande hizo mbili vinaendelea kupigana,

Serikali hizo mbili hasimu ziliibuka mwaka 2014 ambapo moja ina makao yake mjini Tobruk, mashariki mwa nchi na inaungwa mkono na Jenerali muasi Khalifa Haftar, na nyingine ni Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na ambayo inasimamia maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo ukiwemo mji mkuu, Tripoli.

Hivi sasa, licha ya jitiahda zote za kuboresha hali ya mambo, Libya inakabiliwa na vita vya ndani na uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi wa madola ya kigeni. Khalifa Haftar ambaye anaongoza wapiganaji wanaojiita, "Jeshi la Kitaifa la Libya', alitembelea Misri Disemba 30 ambapo alizitaka nchi za Kiarabu zichukue hatua ya kuzuia Uturuki kuingia kijeshi nchini Libya.

Haftar aidha ametoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua ya kuzuia kutumwa askari wa Uturuki nchini Libya ili kuzuia kile alichodai ni 'kuporwa utajiri wa Libya."

Safari ya Haftar nchini Misri imefanyika wakati ambao wapiganaji anaowaongoza wanatekeleza mashambulizi dhidi ya Tripoli nayo serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ikiwa imeomba msaada wa kijeshi kukabiliana na wapiganaji hao wa Haftar. Pamoja na kuwa Umoja wa Mataifa unaitambua rasmi serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya, serikali za Misri, Saudi Arabia na Imarati (UAE) zinamtambua jenerali muasi Khalifa Haftar na kumuunga mkono kwa hali na mali katika vita vyake dhidi ya serikali ya Al Sarraj.

Serikali ya Bunge la Tobruk ambayo inapata himaya ya kijeshi ya Haftar mbali na kuungwa mkono na Saudia, Misri na Imarati pia inaungwa mkono na Ufaransa na Russia. Nayo Serikali ya Muafaka wa Kitaifa yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli inaungwa mkono na Uturuki, Qatar na Italia. Weledi wa mambo wanasema hali hiyo ya mambo imepelekea mgogoro wa nchi hiyo kuwa mgumu sana. Hali imekuwa ngumu zaidi hasa baada ya Uturuki kutangaza kuwa itaingilia moja kwa moja katika vita vya ndani ya Libya kwa maslahi ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa. Hatua hiyo ya Uturuki itapelekea mlingano wa nguvu katika nchi hiyo kuvurugika na atakayepata hasara kubwa ni Haftar.

Waziri Mkuu wa Libya wa  Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) Fayez al Saraj (kushoto) akiwa na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

Waziri wa Ulinzi wa Uturuk Hulusi Akar siku ya Jumapili alitangaza kuwa nchi yake iko tayari kutuma askari nchini Libya na kuongeza kuwa hatua hiyo itakuwa na lengo la 'kuunga mkono maslahi ya ndani na ya nje'.  Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki naye alitangaza wiki iliyopita kuwa nchi yake iko tayari kutuma vikosi vya nchi kavu, majini na angani ili kuiunga mkono serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya. Alisema Waziri Mkuu Fayez al Sarraj ameiomba rasmi Uturuki kutuma jeshi ili kuzuia mji mkuu Tripoli kutekwa na wapiganaji wa Haftar. Tovuti ya Al Arabia imedai kuwa serikali ya Uturuki inalenga kutuma wapiganaji elfu nane kutoka Syria waisaidie serikali ya Muafaka wa Kitaifa. Uamuzi wa Uturuki kutuma wanajeshi Libya umepingwa vikali na Misri na Imarati kiasi kwamba Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ameitaka Marekani ifanye inaloweza kuzuia wanajeshi wa Uturuki kuingia Libya. Duru zinadokeza kuwa, Jumanne 31 Disemba, wanajeshi wa Misri na Imarati waliingia Libya wakiwa na zana za kivita ili kuwaunga mkono wapiganaji wanaoongozwa na Haftar na ambao wanalenga kuindoa madarakani serikali ya Fayez al Sarraj ambayo inaungwa mkono rasmi kimataifa. Wanajeshi hao wa Imarati na Misri wameingia Libya ili kubadilisha mlingano wa nguvu kwa maslahi ya wapiganaji wanaoongozwa na Haftar.

Katika upande mwingine, inatarajiwa kuwa katika kipindi cha siku chache zijazo Uturuki itachukua uamuzi kuhusu kiwango cha uingiliaji wake wa kijeshi nchini Libya kwa lengo la kuiunga mkono Serikali ya Muafaka wa Kitaifa. Inasubiriwa kuona iwapo Uturuki itazingatia mistari miekundu  au  inalenga kuingia katika vita kamili ili kuimarisha satwa yake Afrika Kaskazini na mashariki mwa Bahari ya Mediterranea. Kwa maelezo hayo hivi sasa mgogoro wa Libya umebadilika na kuwa mgogoro wa kimataifa ambapo serikali mbili hasimu zinaalika nchi za kigeni ili kutumia nguvu za kijeshi kuushinda upande wa pili.

Jenerali muasi Libya Khalifa Haftar (kushoto) akiwa na Mfalme Salman wa Saudi Arabia

Hitajio la kimsingi kabisa la vikosi vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya katika vita vya sasa ni kupata nguvu za kijeshi angani ili kuzuia mji wa Tripoli kudondoshewa mabomu na jeshi la Hafta. Kwa kuzingatia kuwa Haftar anapata himaya ya ndege za kivita za Misri na Imarati, iwapo Uturuki itatuma ndege zake za kivita aina ya F-16 basi nukta hiyo itapelekea vikosi vya nchi kavu vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa kupata nguvu zaidi ya kukabiliana na wapiganaji wa Haftar. Iwapo kuingia Uturuki kijeshi nchini Libya kutapelekea tu kulindwa serikali ya Tripoli na kuhakikisha  inabakia madarakani, basi kuna uwezekano  kuwa Misri na Imarati zitajizuia kuingia katika vita vya moja kwa moja na Uturuki. Lakini iwapo kuingia Uturuki vitani Libya kutapelekea kurudi nyma wapiganaji wa Haftar na kusonga mbele askari wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa kwa lengo la kuchukua udhibiti wa eneo la mashariki mwa Libya, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa majeshi ya Misri na Imarati yataingia vitani moja kwa moja.

Kwa msingi huo, kuna uwezekano kuwa mgogoro wa sasa wa Libya utageuka na kuwa mapambano makubwa baina ya madola kadhaa ya kigeni katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tags