Misri yatahadharisha kuhusu madola ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Libya
(last modified Mon, 03 Feb 2020 03:06:48 GMT )
Feb 03, 2020 03:06 UTC
  • Misri yatahadharisha kuhusu madola ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Libya

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ametahadharisha kuhusu madhara yanayosababishwa na madola ajinabi ya kuingilia masuala ya ndani ya Libya.

Balozi Hamdi Sanad Loza ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri katika Masuala ya Afrika alisema hayo jana (Jumapili) akisisitiza kuwa, uharibifu ndiyo matunda pekee ya uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya.

Aidha amesisitiza kwa kusema, uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Libya umeharibu utulivu na usalama si wa Libya pekee bali pia wa nchi jirani na kwamba machafuko yanayoendelea Libya ni madhara kwa usalama wa eneo zima la Sahel.

Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja tangu mwaka 2011

 

Naibu huyo wa waziri wa mambo ya nje wa Misri ametoa mfano kwa kusema, miongoni mwa hatua haribifu zinazofanywa na madola ajinabi ni kuhamishwa magaidi wanaofanya jinai Syria na kupelekwa Libya.

Machafuko nchini Libya yalipamba moto kuanzia mwezi Aprili 2019 baada ya jenerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha vita vikubwa vya pande zote dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa nia ya kuinganusha serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj na ambayo ndiyo inayotambuliwa na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.

Jenerali muasi Khalifa Haftar anaungwa mkono kikamilifu na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi hasa Ufaransa, wakati serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo ikiungwa mkono pia na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ambaye hata ametuma wanajeshi wake Libya kwenda kuisaidia serikali ya Fayez al Sarraj.

Tags