PLO yaitahadharisha Sudan isifanye uhusiano na utawala haramu wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59350-plo_yaitahadharisha_sudan_isifanye_uhusiano_na_utawala_haramu_wa_israel
Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ameitahadharisha Sudan kuhusu jitihada zake za kutaka kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 24, 2020 03:05 UTC
  • Saeb Erekat
    Saeb Erekat

Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ameitahadharisha Sudan kuhusu jitihada zake za kutaka kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Saeb Erekat amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Utawala nchini Sudan, Abdel Fattah al-Burhan kushikamana na mpango wa amani uliopendekezwa na nchi za Kiarabu, asifanye suluhu na Israel na aelewe mashaka ya taifa la Palestina yanayosababishwa na uvamizi na mzingiro wa utawala wa Kizayuni. 

Mapema mwezi huu wa Februari Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alikutana na kufanya mazungumzo na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Uganda. Hatua hiyo ya al Burhan imelaaniwa vikali ndani na nje ya Sudan. 

Image Caption

Siku mbili baadaye ndege ya abiria ya Israel ilipita kwa mara ya kwanza katika anga ya Sudan ikiwa njiani kuelekea Kinshasa. 

Chama cha Wananchi cha Congress nchini Sudan kilitoa taarifa kikisema: "Mkutano wa Al Burhan na Netanyahu nchini Uganda unaenda kinyume na msimamo wa watu wa Sudan wa kuunga mkono Wapalestina katika mapambano yao na utawala ghasibu wa Israel." 

Vilevile Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amekosoa vikali hatua hiyo na kusema kuwa, uamuzi wowote kuhusu masuala ya nje ya Sudan unapaswa kuchukuliwa na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na wala sio mtu binafsi.